Ministry of Health, Community Development, Gender, Elderly and Children

KONGAMANO NA MKUTANO MKUU WA WATAALAMU WA MAENDELEO YA JAMII

TAREHE 21 HADI 24 OKTOBA, 2019

DODOMA CONVENTION CENTRE.

Fanya Usajili

1.0 UTANGULIZI

Wizara ya Afya (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) tangu mwaka 2001 imekuwa ikifanya Mkutano Mkuu wa Watalaamu wa Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi katika kutekeleza majukumu ya Sekta ya Maendeleo ya Jamii. Mikutano 13 imekwishafanyika na kuhudhuriwa na Wataalam wa Kada ya Maendeleo ya Jamii kutoka Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi za Wizara na Wizara za kisekta na Asasi za Kiraia.

Mkutano wa 13 ulikuwa tofauti na mikutano mingine iliyopita ambapo uliongeza wigo wa ushiriki kwa kuhudhuriwa na Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kutoka Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi kama vile Makampuni, Ajira Binafsi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu. Pili, washiriki walilipa gharama za kuhudhuria Mkutano. Tatu, maandalizi ya Kongamano yalishirikisha wadau hususani Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA). Hivyo, Mkutano wa 14 unaoandaliwa umezingatia uzoefu, fursa na changamoto zilizojitokeza katika mikutano iliyopita hasa Mkutano wa 13 nia ikiwa ni kuboresha zaidi.

2.0 UMUHIMU WA KONGAMANO NA MKUTANO

Kongamano na Mkutano huu ni muhimu kwani utawakutanisha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii ili kupeana mbinu na mikakati itakayowezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha zaidi. Pia, Mkutano utatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na mbinu mpya zinazoibuka katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika jamii.

3.0 LENGO KUU LA KONGAMANO NA MKUTANO

Kubadilisha uzoefu na Kujengeana uwezo wa kuimarisha huduma za Maendeleo ya Jamii.

  3.1 MALENGO MAHUSUSI

  1. Kujadili utekelezaji wa Sera za Sekta ya Maendeleo ya Jamii.
  2. Kuimarisha ushirikiano na kujengeana uwezo wa Kitaalam kuhusu matumizi ya Teknolojia katika kazi za maendeleo ya jamii.
  3. Kupata uzoefu wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya jamii kwa vitendo kutoka katika vyuo vinavyotoa taaluma ya maendeleo ya jamii.
  4. Kufanya Mkutano Mkuu wa tatu wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA).
  5. Kuhabarishana na kujifunza kuhusu amsha ari ya ujenzi wa makazi bora

4.0 MATOKEO YA KONGAMANO NA MKUTANO
  1. Kupata mrejesho wa utekelezaji wa maazimio ya Kongamano na Mkutano Mkuu wa 13
  2. Kupata mbinu za utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kwa kupitia Teknolojia.
  3. Kupata maarifa na uzoefu wa jinsi gani Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vinaoanisha nadharia na vitendo kwa kutumia teknolojia.
  4. Kuimarisha chama cha wanataaluma wa maendeleo ya jamii
5.0 KAULI MBIU

“Maendeleo ya Jamii ni chachu ya mabadiliko chanya katika zama za Teknolojia”

6.0 MAHALI NA TAREHE

Kongamano na Mkutano vitafanyika kwa siku 4 kuanzia tarehe 21 hadi 24 Oktoba, 2019, Dodoma Convention Centre Jijini Dodoma.