Ministry of Health, Community Development, Gender, Elderly and Children

KONGAMANO NA MKUTANO MKUU WA WATAALAMU WA MAENDELEO YA JAMII

TAREHE 26 HADI 29 NOVEMBA, 2018

LUSH GARDEN HOTEL, ARUSHA

Fanya Usajili

1.0 UTANGULIZI

Wizara tangu mwaka 2001 imekuwa ikiandaa Mkutano wa mwaka wa Watalaam wa Maendeleo ya Jamii wenye lengo la kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi katika kutekeleza majukumu ya Sekta ya Maendeleo ya Jamii. Mpaka sasa jumla ya mikutano 12 imeweza kuandaliwa na kuhudhuriwa na wataalamu wa kada ya Maendeleo ya Jamii kutoka Sekretariati za Mikoa , Mamlaka za Serikali za Mitaa , Taasisi za Wizara na Wizara za kisekta.

Mkutano wa 13 unaoandaliwa umezingatia uzoefu wa mikutano iliyopita. Uzoefu huu unaonyesha kuwa kundi kubwa la wataalamu wa Maendeleo ya Jamii nje ya Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mikoa hawapati fursa ya kuhudhuria. Hivyo, Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kutoka Sekta binafsi kama vile Makampuni, Ajira binafsi, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Vyuo na Taasisi za elimu ya juu hawapati fursa ya kuhudhuria na kushiriki mkutano wa sekta. Changamoto kubwa zilizopelekea wataalamu wengi kutokuhudhuria ni pamoja na;

 1. Kutokuwepo kwa mfumo unaowezesha watalaam wote kutoka sekta ya umma na binafsi kushiriki.
 2. Kukosekana kwa chama imara cha wataalamu wa maendeleo ya jamii (profesional association) chenye wanachama kutoka sekta ya umma na binafsi ambacho kingepaswa kufanya maandalizi ya mkutano wa wanachama.

Kwa kutambua changamoto zilizoainishwa, maandalizi ya mkutano wa 13 yanazingatia mambo makubwa mawili;

 1. Kushiriki kwa wadau mbalimbali katika kugharamia kongamano na mkutano.
 2. Wizara kushirikiana na Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii (CODEPATA) katika maandalizi ya kongamano na mkutano.

Hivyo basi, ushirikiano wa Wizara na CODEPATA unapelekea kufanyika kwa Kongamano pamoja na Mkutano Mkuu wa CODEPATA kwa wakati mmoja.

2.0 UMUHIMU WA KONGAMANO NA MKUTANO

Kongamano na mkutano vina umuhimu wa kipekee kwa kuwakutanisha kwa mara ya kwanza Watalaamu wa Maendeleo ya Jamii kutoka sekta binafsi na umma. Aidha, na kuwawezesha kubadilishana uzoefu na mbimu mpya zinazoibuka katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika jamii

3.0 LENGO KUU LA KONGAMANO NA MKUTANO

Kuboresha utendaji kazi kwa kuwashirikisha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kutoka katika sekta mbalimbali

  3.1 MALENGO MAHUSUSI

 1. Kujadili utekelezaji wa Sera za Sekta ya Maendeleo ya Jamii.
 2. Kubadilishana uzoefu wa mbinu mpya za kiutendaji, kujenga uwezo, na kuimarisha ushirikiano wa wataalamu wa Maendeleo ya Jamii.
 3. Kupokea matokeo ya tafiti kutoka Vyuo vinavyotoa taaluma ya Maendeleo ya Jamii.
 4. Kufanya mkutano mkuu wa chama cha kitaaluma cha maendeleo ya jamii Tanzania (CODEPATA).

4.0 MATOKEO YA KONGAMANO NA MKUTANO
 1. Kupata mrejesho wa utekelezaji wa sera za sekta ya maendeleo ya jamii.
 2. Washiriki wa mkutano kushiriki katika shughuli za kijamii mkoani Dodoma.
 3. Utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kupitia matokeo ya tafiti.
 4. Kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa wataalamu wa Maendeleo ya Jamii.
5.0 KAULI MBIU

Kauli mbiu zifuatazo zinazopendekezwa ni;

 1. “Wataalam wa Maendeleo ya Jamii ni Chachu katika kufikia Uchumi wa Kati 2025”
6.0 MAHALI NA TAREHE

Kongamano na Mkutano vitafanyika kwa siku 4 kuanzia tarehe 26 hadi 29 Novemba, 2018, Lush Garden Hotel Mkoani Arusha.